Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge ameyasema hayo jana tarehe 27 Mei 2026 wakati wa maadhimisho ya ibada ya Swala ya Eid Al-Adh-ha iliyofanyika katika Msikiti wa Ghadeer, eneo la Kigogo Post jijini Dar es Salaam, ambapo waumini wengi walihudhuria kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo tukufu.
Katika hotuba yake yenye mawaidha na nasaha muhimu kwa jamii, Sheikh Jalala aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha umoja na kushikamana katika nyakati zote, huku akisisitiza kuwa; mshikamano wa wananchi ndio silaha kubwa ya kulinda usalama, utulivu na mafanikio ya taifa.
Aidha, alieleza kuwa; suala la amani na umoja halipaswi kuangaliwa kwa misingi ya tofauti za kidini, kikabila wala kijamii, bali linapaswa kupewa nafasi ya juu kama tunu ya pamoja inayowahusu wanadamu wote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Sheikh Jalala alisema kuwa; dini mbalimbali zinatufundisha mema, upendo na kuheshimiana, hivyo jamii inapaswa kuishi kwa kusaidiana na kushirikiana ili kujenga taifa lenye maelewano na lenye kuzingatia utu wa kila mmoja.
Akizungumza mbele ya mamia ya waumini waliohudhuria swala hiyo ya Eid, Sheikh huyo alitahadharisha dhidi ya kauli za chuki, migawanyiko na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani ya nchi, huku akibainisha kuwa; jukumu la kuilinda Tanzania ni la kila mwananchi bila kujali tofauti zao.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kuendelea kutumia majukwaa yao kwenye kuhubiri amani, maadili mema na mshikamano wa kitaifa, huku akieleza kuwa; jamii yenye upendo na umoja ndio jamii yenye uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Maadhimisho hayo ya Eid Al-Adh-ha katika Msikiti wa Ghadeer yalifanyika katika hali ya utulivu na mshikamano mkubwa, ambapo waumini walipata fursa ya kusikiliza mawaidha ya kidini yaliyolenga kuimarisha maadili, kuhamasisha upendo miongoni mwa wananchi na kuendeleza tunu ya amani nchini Tanzania.






Maoni yako